Majina ya wasanii ambao wanawania kuingia kwenye tuzo za Rock & Roll Hall of Fame kwa mwaka wa 2021 yametajwa.
Miongoni mwao ni mwanzilishi wa muziki wa Afro Beat kutoka nchini Nigeria, Fela Kuti. Wengine waliotajwa kuwania nafasi ya kupewa heshima hiyo ni rapa Jay-Z, LL Cool J, Tina Turner na wengine kibao.
Rock & Roll ni muziki uliofanya vizuri nchini Marekani kuanzia miaka ya 1940 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1950.
Sasa tangu mwaka wa 1986, kumekuwa na utaratibu wa kuwapa heshima wasanii ambao wamechangia kuleta mageuzi kwenye muziki huo hata kama sio msanii wa aina hiyo ya muziki.
Miaka ya hivi karibuni wasanii wa Hip Hop pia wamekuwa wakipewa heshima kwenye Rock & Roll Hall of Fame kwa sababu inaaminika wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwashawishi wasanii wanaofanya muziki wa Rock kwa sasa.
Watakaofanikiwa kupita kwenye mchujo wa kura wa tuzo hiyo watatangazwa mwezi Mei mwaka huu na Hafla ya kuwatunuku heshima hiyo itafanyika huko Cleveland, Ohio,nchini marekani September mwaka huu.