Bosi wa lebo ya muziki ya Mpaka Records msanii Ykee Benda alijiingiza kwenye majibizano makali na mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii wiki chache zilizopita.
Hii ni baada ya mashabiki kumtaka ashinikize kuachiliwa kwa msanii Nubian Li ikizangatiwa kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa Muungano wa Wanamuziki nchini Uganda.
Msanii huyo alijitokeza na kusema kuwa Nubian Li alikamatwa kama mwanasiasa na hivyo hana mamlaka ya kumtetea. Jambo hilo halikuwafurahisha baadhi ya mashabiki wake ambao walienda mbali zaidi na kuanza kumporomoshea matusi makali.
Mmoja wa mashabiki wake alimshtumu vikali hitmaker huyo wa “Muna kampala” kwa madai ya kuhusika na ubakaji kipindi msanii huyo yupo Shule ya Upili.
Baada ya ukimya wa siku chache, Ykee Benda amejitokeza kupitia mtandao wake wa Kijamii na kukanusha madai hayo huku akiyataja kuwa hayana msingi.
“Kama ilivyozoeleka, mambo mengi yasiyokuwa na staha yalichapishwa mtandaoni ikiwemo madai ya ubakaji yaliyoibuliwa na mmoja wa watumiaji wa Twitter aliyedai ilitokea kipindi nipo shule ya upili. Ningependa kusema kwamba madai hayo hayana msingi na yanapaswa kuchukuliwa kama uvumi usiokuwa na msingi, ”alitweet kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Ykee Benda pia amedai kuwa msimamizi wa akaunti yake ndiye alihusika moja kwa moja kwenye ishu ya kurushiana maneno makali na mashabiki wake na wala sio yeye.