Wawakilishi wadi kaunti ya Turkana wametakiwa kupitisha ripoti ya BBI kwani inapendekeza nyongeza ya ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti ambayo italeta maendeleo mashinani.
Akizungumza kwenye mkutano wa BBI mjini Lodwar Waziri wa Mafuta na Madini John Munyes amesema kuongezwa kwa mgao wa fedha za kaunti kutoka asilimia 15 hadi 35 itachangia pakubwa kuendeleza miradi ya maendeleo kaunti hiyo.
Aidha Munyes ameongeza kuwa pendekezo la kubuniwa kwa hazina ya maendeleo ya wadi katika ripoti ya BBI itachangia katika utekelezwaji wa miradi ya maendeleo mashinani.
Sanjari na hilo ametoa wito kwa serikali ya kitaifa kutoa msaada wa chakula kwa wakaazi wa kaunti ya Turkana ambao anadai wameathirika na makali ya njaa.
Kuhusu suala la usalama mshirikishi wa BBI kaunti ya Turkana Beatrice Asukul ameitaka serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya Usalama wa Ndani kuihimarisha usalama eneo la Kapedo hata baada ya operasheni kukamilika ili kuwaondolea wananchi hofu ya kushambulia tena na majangili.