Wakazi wa eneo Bunge la Kacheliba wametahadharishwa dhidi ya kuharibu misitu kwa kukata miti na kuchoma makaa na wengine kuiuza kwa matapeli wanaodaiwa kusafirisha miti hiyo kutoka eneo hilo na kuivusha nchini jirani ya Uganda bila idhini.
Akizungumza na kituo hiki kwa njia ya simu, Afisa wa misitu katika eneo la Kacheliba Damiano Morlem, amesema miti ya kiasili iko kwenye hatari ya kumalizika iwapo wananchi hawataitunza kikamilifu.
Damiano amesema kumekuwapo na changamoto za kuwakabili wahalifu hao hasa wanaotoka nchini uganda, japo amewaonya kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atayepatikana akikaidi amri hiyo.
Kwa upande wake Meshack Lomang’ura ambaye pia ni afisa katika idara hiyo, amewasihi wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi kuchukua jukumu la kutunza misitu bila kushurutishwa.