Shirikisho la kitaifa la wakulima nchini KENAFF imeweka mikakati ya kuwafikia wakulima wenye ulemavu kwenye kaunti takribani 28 za humu nchini ili kuwasaidia kujikimu wakati huu mgumu wa msambao wa virusi vya corona.
Akizungumza katika kaunti ya Uasin Gishu Afisa Mkuu mtendaji wa KENAFF Daniel Mwenda amesema muungano huo unalenga kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mafunzo ya kilimo bora na fedha za kuwasaidia kujiimarisha hata zaidi.
Aidha Mwenda amesema kwa sasa wakulima hao wamepewa kima cha shilingi elfu mia mbili hamsini kuanzisha miradi na fedha hizo zinatarajiwa kuongezeka kwa awamu ya tatu.
Hata hivyo amesema kwamba walemavu watapewa nafasi ya kuwa wanachama wa bodi ya muungano huo ili kuhakikisha kwamba wanawakilishwa vyema na maswala yao yanaangaziwa kikamilifu.
Tayari wakulima wenye ulemavu wa maeneo mbalimbali wamekumbatia mbinu za kilimo tofauti kama vile ufugaji wa mbuzi, upanzi wa ndizi na hata utengenezaji wa vyakula vya mifugo.