Siku moja tu baada ya kaunti kamishna kaunti ya Turkana Muthama Wambua kudai kuwa serikali ya kaunti ya Turkana imemsurutisha atekeleze agizo la kuingia na kutotoka kaunti hiyo, naibu gavana kaunti hiyo Peter Lotethiro amejitokeza na kukana madai hayo.
Kulingana na Lotethiro serikali ya kaunti ilipendekeza serikali kuu iweke mikakati zaidi ya kuwalinda wananchi wake dhidi ya maambukizi ya corona ila sio kufunga mipaka ya kaunti ya Turkana kama ilivyoripotiwa.
Aidha Lotethiro amesisitiza haja ya madereva wa magari ya masafa marefu wanaoingia kaunti ya Turkana kuwa na vyeti vya kuonyesha hawana maambukizi ya virusi vya corona akisema ni mojawapo ya mikakati iliyowekwa na kamati iliyobuniwa kukabiliana na janga la corona kaunti hiyo.
Wakati uo huo ametetea serikali ya kaunti ya Turkana dhidi ya hatua ya kuwazuilia madereva wa masafa marefu katika maeneo ya Nadapal akisema ni jukumu ya serikali kuwalinda wakaazi wake dhidi ya maambukizi ya ugojwa wa COVID-19 baada ya madereva sita kuripotiwa kuwa na maambukizi ya virusi hivyo.
Kauli yake imetiliwa mkazo na Waziri wa Afya kaunti ya Turkana Jane Ajele ambye amewataka wakaazi wa kaunti hiyo kutilia manani masharti ambayo yamewekwa na Wizara ya Afya ili kukabili maambukizi ya virusi vya Corona.
Hata hivyo baadhi ya madereva ambao wamewekwa karantini katika eneo la Nadapal mpakani mwa Kenya na Sudan Kusini wanalalamikia jinsi serikali imejikokota kwenye swala la kuwashughulikia ili kuwaruhusu kuendelea na safari zao.