Rais wa klabu ya Fenerbahce, Ali Koc amewataka mashabiki wa timu hiyo kuchangia mshahara wa Mesut Ozil baada ya fundi huyo wa mpira kujiunga kwenye kikosi chao.
Ozil alitangazwa rasmi juzi kujiunga na miamba hiyo ya soka Uturuki ambapo amesaini mkataba hadi 2024. Ozil alikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa wakilipwa mshahara mkubwa Arsenal, Pauni 350,000 kwa wiki.
Hata hivyo, wakati akipunguza mshahara wake kwa asilimia 80 ili tu kwenda kujiunga na Fenerbahce, kiasi kilichobaki bado kinaonekana kikubwa kwa wakali hao wa Super Lig.
Kwa mujibu wa goal.com, kinachoelezwa ni kwamba Ozil sasa atakuwa akilipwa Pauni 67,000 kwa wiki, ikiwa ni sawa na Pauni 3.5 milioni kwa mwaka.
Katika kumudu gharama za mshahara wa staa huyo, Koc amewaomba mashabiki kuchangia.