Msanii wa Kundi maarufu la ‘Longombas’ kutoka Kenya Christian Longomba amefariki dunia, imeripotiwa kuwa umauti umemkuta katika Hospitali huko Los Angeles nchini Marekani akipatiwa matibabu.
Chanzo cha kifo chake kinatajwa kuwa ni ugonjwa wa uvimbe kwenye ubongo wake ‘brain tumor’ ambao amekuwa akipambana nao kwa muda wa miaka mitano sasa.
Mwezi Mei mwaka wa 2015, Christian aligundulika kuwa na uvimbe kwenye ubongo na alifanyiwa upasuaji kuuondoa. Upasuaji huo ulienda vyema lakini ilibidi apasuliwe tena mara baada ya madaktari kubaini kuganda kwa damu kwenye ubongo.
Kifo cha Christian kimethibitishwa na kaka’ke ambaye pia ni mwanamuziki mwenza Lovi Longomba. “Nakupenda Kaka yangu, Partner wangu na Rafiki yangu lakini Yesu amekupenda zaidi, uwe na furaha mbinguni” – ameandika Lovy.
Wawili hao ambao ni wapwa wa mwanamuziki Awilo Longomba walianza Muziki wakiwa nchini Kenya miaka ya 2000. Kundi la Longombas lilitamba na nyimbo kama vuta pumzi, shika more na dondosa.
Baadaye walihamia Marekani ambapo waliachana na muziki wa dunia na kuwa wahubiri wa injili.