Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini Anne Nderitu atavifutia usajili Vyama vya Siasa ambavyo shughuli zao zitakumbwa na ghasia kuelekea wakati wanapojiandaa na Uchaguzi Mkuu wa 2022.
Nderitu amevitaka Vyama ambavyo wanachama wao walihusika katika ghasia zilizozikumba Chaguzi ndogo katika maeneo ya Bunge na Wadi kadha wiki jana vijisafishe.
Kulingana na kipengele cha 91 cha Katiba, Vyama vya Siasa havipaswi kuhusishwa au kushiriki katika fujo, kwa kutoa vitisho au kushambulia Wanachama wa Vyama vingine.
Pia, havipaswi kushiriki ufisadi, kupokea au kutumia pesa haramu na kutumia rasilimali za Umma isipokuwa fedha ambazo zimetengewa kupitia hazina ya Vyama vya Siasa.