Shirika la afya ulimwenguni WHO limeyahimiza mataifa yanayotumia chanjo dhidi ya corona aina ya Astrazeneca kuendelea kuitumia licha ya baadhi ya mataifa kusitisha matumizi yake.
Kulingana na mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus, kufikia sasa hakuna ushahidi kwamba chanjo hiyo inasababisha mgando wa damu kama inavyodaiwa.
Ameongeza kuwa hata katika mataifa ambayo yamesitisha matumizi ya Astrazeneca idadi ya wanaolalamikia mgando wa damu ni ndogo mno.
Kwa upande wake mtafiti mkuu wa WHO Soumya Swaminathan anasema utafiti unaendelea kuhusu swala hilo na hakuna haja ya watu kuwa na hofu.