Mahakama kuu ya Kitale hii leo imeamuru kusitishwa kwa shughuli zozote za kuhifadhi wanyama pori zinazoendeshwa na shirika la kibinafsi la NRT, katika shamba la ekari elfu 250 katika wadi sita za kaunti ya Pokot Magharibi.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Mwangi Njoroge ametaka upande wa walalamishi na wahojiwa kusubiri uamuzi wa mahakama hiyo mnamo machi 16 ili kuendeleza shughuli katika shamba hilo na kusitisha shughuli za kuwafurusha wakazi kutoka mashamba hayo.
Wakazi 550 walielekea mahakamani kwa niaba ya ya wakazi alfu 70 kusitisha shughuli hizo kwa vigezo kuwa wananchi wamenyimwa haki kwani hawakuhusishwa kutoa maoni yao kwa shamba hilo kutwaliwa, na shirika la Northern Rangeland Trust chini ya ufadhili wa umoja wa ulaya, katika shughuli za kuhifadhi mazingira, mifugo, na wanyama pori.
Shirika la NRT lilikua na mkataba wa maelewano kati ya serikali ya kaunti ya pokot magharibi, kutwaa mashamba hayo ya kijamii kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2014 hadi 2024 katika wadi za Seker, Lomut, Kasei, Masol, Weiwei na Endugh maeneo bunge ya Sigor na Kacheliba, kaunti ya Pokot Magharibi.