MAAMBUKIZI YA UGONJWA WA UKIMWI YAPUNGUA TURKANA

MAAMBUKIZI YA UGONJWA WA UKIMWI YAPUNGUA TURKANA

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Turkana Jane Ajele amesema visa vya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi miongoni mwa wakaazi kaunti hiyo vimepungua kwa asilimia kubwa.

Akizungumza Mjini Lodwar kwenye hafla ya kutathmini utendakazi wa shirika la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation ambalo linasitisha shughuli zake Kaunti ya Turkana, Ajele amesema maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi yamepungua kutoka asilimia 7.2 hadi asilimia 3.2 akisema kuna imani ya kurudisha asilimia hiyo ya maambukizi hadi asilimia sifuri.

Aidha,Ajele amepongeza shirika la EGPAF kwa utendakazi wake kwa muda ambao wamehudumu Kaunti ya Turkana kwani kwa sasa kuna vituo vitatu vya afya ambavyo vimebuniwa kupima na kutoa ushauri kwa waathiriwa wa ugonjwa wa Ukimwi,akiwataka wakaazi kujitokeza kupima na kujua hali zao.

Kauli sawa imetolewa na baadhi ya wakaazi wa Kaunti ya Turkana waliofaidi na  Shirika la EGPAF ambao wamesema wamefurahishwa na huduma bora ambayo shirika hilo limekuwa likitoa kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kaunti hiyo.

Hata hivyo Ajele amedokeza kuwa shirika la AMPATH sasa litachukua rasmi nafasi na majukumu ambayo yamekuwa yakitolewa na shirika la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation ambalo linasitisha shughuli zake Kaunti ya Turkana baada ya mwongo mmoja huku akisema wahudumu 300 wa Afya ambao wamekuwa wakihudumu na EGPAF watapewa  ajira na shirika la AMPATH.

 

Write a Message

Your email address will not be published.

Related Posts