Rais Joe Biden wa Marekani amezungumza kwa simu na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ikiwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kujadiliana kuhusu ushirikiano.
Hata hivyo hayakuwa mazungumzo ya kawaida baada ya kusogezwa mbele kwa takriban mwezi mmoja, tofauti na huko nyuma ambako viongozi wa mataifa hayo huzungumza katika kipindi cha siku chache baada ya kuingia madarakani.
Kusogezwa mbele kwa mazungumzo hayo kuliibua madai kwamba Biden alikuwa akikwepa kuzungumza na Netanyahu kutokana na ukaribu wake na mtangulizi wa Biden, Donald Trump.
Kwenye ukurasa wake wa twitter, Biden amesema wamekuwa na mazungumzo ya kirafiki na ucheshi ya karibu saa moja na kusema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano thabiti baina ya mataifa yao.
Kulingana na Ikulu ya White House, Biden alitilia mkazo masuala ya ushirikiano wa kijeshi, kurejesha mahusiano kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu na Kiislamu katika hali ya kawaida na kusaka amani ya kikanda, hususan kati ya Israel na Palestina