Mchekeshaji maarufu nchini Eric Omondi amemuomba msamaha Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Uainishaji wa Filamu nchini Ezekiel Mutua.
Eric amethibitisha kuomba msamaha kupitia akaunti yake ya Instagram baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 50 jana, siku moja baada ya kukamatwa kwa makosa ya jinai.
Mchekeshaji huyo alikamatwa Machi 11 mwaka huu kwa kukiuka sheria ya maadili katika utengenezaji na maonyesho ya filamu kwa kipindi chake cha ‘Wife Material’.
Eric omondi amekubaliana na Mutua baada ya kufanya naye mazungumzo kwa njia ya simu kuwa kipindi chake hicho hakihitaji kuwa na mahudhui yasiyofaa ili kupata wafatiliaji.
Pia Eric omondi amewaomba radhi watu wote aliowakwaza kwa namna yoyote kupitia kipindi chake hicho alichokitaja kuwa anakitumia kuiunganisha Afrika mashariki kupitia Burudani.